#MzeeWangu

Mzee wangu, natumai hapo ulipo pema,
RIP, afadhali wewe ulishaenda mapema,
Kwa sababu yale ungeyaona leo mate lazima ungeyatema,
Juu wanayoyafanya wako serious lakini ungedhani wanakupima,
Samahani mzee, sikuandikii kukubebesha lawama,
Nataka ujuwe sisi ulotuacha nyuma,
Mandumakuwili hatuna mbele wala nyuma.

Dunia ya sasa imejawa vioja,
Vya ghali utavipata kwenye toja,
Warembo wa kwetu kazi wanafanya ni kuonjaonja,
Roho walishazigeuza ngumu kama za soldier.

Wanauza sura ndo wanaume wetu wanunue ngono,
Wao nao hawatosheki na wake zao kuna za uchi ziuitwa pono,
Ndo wakirudi nyumbani performance ka konokono,
Tofauti ni fikra zao zenye mbio kama Kiprono,
Kisha maswali yanaibuka eti kilitoka wapi kisonono.

Wasichana uliowaacha walikuwa na kipaji,
Kuchanja kuni na hata mtoni kuchota maji,
Maneno machafu katu walikuwa hawataji,
Kwa watoto walijua kufanya upakataji,
Siku hizi hao hushindana kuwa majimaji,
Kaa la moto kwenye kidonda washageuka wasagaji,
Hawazungumzii mambo haya kama vile ubakaji,
Na swala la wanaume wawili kugandana kama maji na saruji.

Mzee wangu, wake zetu walishatupa talaka,
Nadhani huko uliko ushaskia binadamu mnyama anabaka,
Ama mwingine sehemu zingine mafuta anapaka,
Ama pia kila kirembo kikipita anataka,
Na akishapata anakigeuza takataka,
Na kukiacha kama mimba ndo mpira ashadaka,
Na moyo wake pia kama mboga ashaukatakata,
Tabia hizi kweli mzee ni za walotakata?

Mzee, huku niliko dada zetu mimba wanatoa,
Na malipo ya kutoa waume wao ndo wamewapea,
Si halali mzee hilo bado hawajatambua,
Ni dhambi kwa mwenye enzi nilidhani wanajua,
Isitoshe ngozi zao hawataki kuridhia,
Maisha ya wale wa juu wanataka kukaribia,
Wanataka kuwa theluji kwa hivyo wanachibua,
Sauti yao yabusu hadi hujui ukunekune au kupapasua.

Mzee wangu, ulotuacha tulikuwa waswahili wa Pemba,
Wenye nyoyo nyeupe ungedhani pamba,
Na sasa naona hatujuani kama tushavua vilemba,
Walio nazo wanakula na kusaza huku wenzao hawana hata cha kulamba,
Wamekonda kama kamba,
Huku wao wamejaa utadhani mamba,
Ni kweli utu kwao umekuwa haba,
Na ndo maana hata kwa mapenzi hakuna mahaba,
Hakuna yeyote anayetambua njia ya msalaba,
Na wale wanaotambua ujuzi wao bado ni bapa,

Chuki nimezoea ni kati ya mbwa na paka,
Paka na panya,
Panya na nyoka,
Nyoka na binadamu,
Ila hii kati ya binadamu na binadamu,
Bado kuijua nina hamu.

Kuna wakati ulituambia kuwa akili ni nywele,
Ila tunavyojuwa saa hii ni kuwa nyinyi wazee ni yaliyopita si ndwele,
Kwa kweli mzee haya mapuuza yamezidi uwele,
Kama vile wanasiasa wametufunza kulipiza kisasi,
Sauti za daku za kina mama zimenyamazishwa na risasi,
Tumelazimishwa kuasi zetu hasasi,
Tulizoletewa nyepesi tumezinatia upesi,
Zimetufanya tuamini ujana ni moshi,
Ndo manake vijana wanachopuliza na kupumua ni moshi,
Mzee wangu si haya yatatuletea mikosi?
Tafadhali huko uliko tuombee tupate nafasi.

Author: sander_ochy

I am a journalist, a poet, a spoken word artist, a writer, and performer. Life is all I write about. #Freeverse254

2 thoughts on “#MzeeWangu”

Leave a reply to Brothers Campfire Cancel reply